Mkutano wa Dondoo 2026 ulifanyika Filomena, Bomang’ombe, ukiwakutanisha wanachama wa Tarafa ya Masama.
Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Dondoo kwa Wanachama 2026
HAI RURAL TEACHERS SACCOS ilifanya Mkutano wa Dondoo kwa wanachama wa Tarafa ya Masama tarehe 7 Septemba 2026 katika Ukumbi wa Filomena, Bomang’ombe.
Katika mkutano huo, wanachama walipata fursa ya kupata mafunzo mbalimbali, ikiwemo mafunzo kuhusu afya ya akili yaliyotolewa na Dkt. Pascal Daniel Kang’iria, mafunzo ya TEHAMA, pamoja na elimu kuhusu bidhaa na huduma zinazotolewa na Chama. Wanachama pia walipatiwa taarifa mbalimbali kuhusu Chama na kupata fursa ya kutoa maoni yao kuelekea Mkutano Mkuu wa Mwaka 2026.
Akizungumza katika mkutano huo, Meneja wa Chama, Upendo Lyatuu, alisema HRT SACCOS imepata mafanikio makubwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo imeongeza wanachama wapya 659. Aidha, mali za Chama zimeongezeka kutoka TSh bilioni 18.7 mwaka 2024 hadi TSh bilioni 21.8 mwaka 2025.
Naye Mwenyekiti wa HRT SACCOS, Mwl. Alex Warioba, akifungua mkutano huo, aliwasisitiza wanachama kujiandaa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi unaofuata kwa kuchagua viongozi bora watakaoliongoza Chama kwa uadilifu na kuleta maendeleo zaidi.
Akifunga mkutano huo, Afisa Ushirika wa Wilaya ya Hai, Paul Ndulu, aliwasisitiza wanachama kuzingatia na kutekeleza mambo yote yaliyojadiliwa katika mkutano huo, pamoja na kuendelea kuwa waadilifu na waaminifu kwa Chama chao.